KATIBU
Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, amepongeza
chama hicho kwa kukata jina la Edward Lowassa, katika kundi la wawania
urais wa chama hicho kwa kuwa hakuwa na sifa za kuwa Rais.
Makamba
amesema hayo jana katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, alipopewa
nafasi ya kusalimia wananchi wa Morogoro, ambapo aliamua kutoa baadhi ya
siri ambazo hazijawekwa hadharani.
Alimtuhumu
Waziri Mkuu huyo wa zamani kwa ufisadi wa kupora ranchi za taifa katika
mikoa ya Tanga na Arusha na kumpatia zabuni zote dada yake katika
Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, ambako Lowassa alikuwa mbunge.
Akizungumzia
madai ya Lowassa kwamba anachukia umasikini wa Watanzania, Makamba
alisema Lowassa hachukii umasikini wa Watanzania, bali anachukia
umasikini wa kwake na ndio maana hajaacha kujilimbikizia mali.
Makamba
alidai kuwa Lowassa alipokuwa Waziri wa Maji na Mifugo, alipora
iliyokuwa Ranchi ya Taifa ya Mkata iliyopo Tanga, ambayo imezungukwa na
vijiji vya Tototwa, Mabwegere, Kiduhu na Tambara.
Katibu
Mkuu huyo alihoji kama Lowassa alikuwa na uchungu na wananchi, kwa nini
hakuwapa wananchi wa vijiji hivyo, badala yake akaichukua yeye na
rafiki yake aliyedai ni wa Hoteli ya Nam.
Ranchi
ya pili anayodaiwa kuipora ni ya Mzeri iliyopo Wilaya ya Handeni mkoani
Tanga, ambayo Makamba alidai kuwa ranchi hiyo iliyokuwa ya Ushirika,
Lowassa aliipora na ina ng’ombe ambayo akiitembelea hawezi kuimaliza
bila kutumia helkopta.
Makamba
alikwenda mbali zaidi na kusema mkoani Arusha wakati akiwa Katibu
Mtendaji wa CCM, Lowassa alipora tena ranchi nyingine ya Leteni.
Mbali
na uporaji huo wa ardhi, Makamba alisema Lowassa pia amempa dada yake,
ambaye hakumtaja jina, zabuni zote za Halmashauri ya Wilaya ya Monduli,
mpaka zabuni za kuiuzia halmashauri hiyo penseli.
Baada
ya kutoa tuhuma hizo, Makamba alisema ameweka akiba maneno mengine na
kumtaka Lowassa, atoke hadharani aseme hayo ili na yeye Makamba ajibu
mahali pengine.
Alisema
Lowassa alitaka kujitoa CCM mwaka 1995 wakati alipokatwa katika
kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais wa CCM mkoani Dodoma.
Makamba
alidai kuwa walipokwenda katika kikao cha NEC ambacho kilihudhuriwa na
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alihoji kwa nini jina la Lowassa
halikuletwa miongoni mwa wagombea watano wenye sifa.
“Nilijibiwa
Lowassa ni kijana mdogo, lakini ana utajiri mkubwa ambao haujulikani
alikoupata. Nikauliza ameulizwa nikajibiwa hapana nikasisitiza aulizwe
maana ndio utaratibu wa chama. Lakini Mwalimu Nyerere alinijibu Lowassa
akija muulize wewe mwenyewe.
“Lowassa
alipoingia katika kikao, nikaitwa Makamba ulikuwa na hoja, nikasimama
nikamwambia bwana wewe Lowassa umekatwa jina lako kwa kuwa una utajiri
ambao haujulikani ulipoutoa,” alidai Makamba.
Kwa
mujibu wa madai ya Makamba, Lowassa alijibu kuwa ni kweli ana utajiri
lakini ni kama wa watu wengine na alishindwa kutoa maelezo ya kutosha
kuhusu alikotoa mali hizo.
Credit:Mpekuzi
Post a Comment