Timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ imefanikiwa kutinga Fainali
ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki maarufu kama CECAFA Challenge
baada ya kuwachapa mabingwa watetezi, Uganda mabao 2-1, jioni ya leo
Uwanja wa Moi mjini Kisumu, Kenya.
Zanzibar sasa itakutana na wenyeji, Kenya kwenye mchezo wa fainali
Jumapili Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos, hayo yakiwa marudio ya
mchezowa Kundi A uliomalizika kwa sare ya 0-0 Desemba 9.
Kenya walitangulia fainali jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Burundi
kwenye Nusu Fainali ya kwanza iliyodumu kwa dakika 120, baada ya dakika
90 kumalizika timu hizo zikiwa hazijafungana.
Abdulaziz Makame Hassan alianza kuifungia Zanzibar Heroes dakika ya 22
akimalizia kona ya chini chini ya beki, Adeyoum Ahmed Seif ambayo mabeki
wa Uganda walizembea kuokoa hadi mchezaji huyo akageuka na mpira na
kufunga. Baada ya bao hilo, kocha wa Uganda, Moses Basena alifanya
mabadiliko akimtoa beki Shafiq Bakari na kumuingiza Joseph Nsubuga
dakika ya 26.
Na dakika mbili baadaye, Uganda wakasawazisha bao hilo kupitia kwa
Derrick Nsibambi aliyefunga dakika ya 28 akimalizia krosi ya Allan
Kyambadde.
Kipindi cha pili timu zote zilianza kwa kusukuma mashambulizi na mchezo
ukazidi kuchangamka, lakini bahati ilikuwa ni ya Wazanzibar jioni ye leo
baada Mohamed Issa ‘Banka’ kumtungua kipa Ismail Watenga dakika ya 57
kwa mkwaju wa penalti na kuipatia Heroes bao la pili baada ya Ibrahim
Hamad Ahmada ‘Hilika’ kuangushwa na Nsubuga Joseph ndani ya boksi dakika
ya 55.
Refa Twagirumukiza Abdoul Karim alimtoa kwa kadi nyekundu Nsubuga kwa
rafu aliyomchezea Hamad Hilika na Korongo wa Uganda wakaanza kurukaruka
kinyonge tangu hapo. Zanzibar wakawa huru mno uwanjani baada ya kadi
hiyo, ingawa dakika za mwishoni walilazimika kucheza kwa kujihami na
kupoteza muda ili kuulinda ushindi wao.
Kikosi cha Uganda kilikuwa; Watenga Ismail, Bernard Muwanga, Shafiq
Bakari/Joseph Nsubuga dk26, Aggrey Madoi, Nicholas Wadada, Tadfeo
Lwanga, Allan Kyambadde/Nelson Senkatuuka dk68, Milton Kalisa, Derrick
Nsibambi, Hood Kawesa na Muzamil Mutyaba/Alan Katerega dk59.
Zanzibar; Mohammed Abulrahman Mohamed ‘Wawesha’, Ibrahim Mohamed/Ibrahim
Abdallah dk87, Adeyum Ahmed, Abdallah Kheri, Issa Haidari, Abdulaziz
Makame, Mohamed Issa ‘Banka’, Mudathir Yahya, Ibrahim Hamad ‘Hilika’,
Feisal Salum/Mohammed Othman dk64 na Suleiman Kassim ‘Seleembe’.
Post a Comment