Ndg. Lowassa akihudhuria ibada katika kanisa la Kilutheri (KKKT) mjini
Tabora amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya
kijamii akidai kuwa, kwa kuwa toka nchi ipate uhuru hajawahi kutokea
Rais kutoka dhehebu la Kilutheri hivyo mwaka huu ni zamu ya Walutheri.
Chama Cha Mapinduzi kinalaani matumizi ya lugha zinazoligawa Taifa letu
kwa misingi ya udini, ukanda, ukabila na ubaguzi wa aina yeyote kisa tu
kutafuta madaraka.
Kauli hii ya Ndg. Lowassa licha ya kuwa ni kinyume na Sheria za Uchaguzi
za nchi yetu, kinyume na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zilizosainiwa na
vyama vyote, lakini ni kinyume kabisa na mila na desturi za Kitanzania
katika kuhakikisha Taifa hili linabaki kuwa Taifa moja lenye umoja,
amani na mshikamano.
Kwa mfano, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka
2015, yaliyotolewa na Tangazo la Serikali Na. 294 la tarehe 27/7/2015
chini ya kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343,
ukurasa wa 5 kifungu 2.1(k) kinasema:-
"Viongozi wa vyama vya siasa, wagombea au wafuasi wao wahakikishe kuwa
majengo wanayotumia kufanya kampeni sio ya Ibada. Vile vile, vyama vya
siasa vihakikishe kuwa havitumii viongozi wa dini kupiga kampeni kwa
ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao".
Lakini katika maadili hayo hayo, ukurasa wa 7, kifungu 2.2(i) kinasema:-
"Vyama vya siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya UDINI, UKABILA, JINSIA AU RANGI."
Kwa kuwa Ndg. Lowassa siku hizi tabia ya kusahau inaongezeka kwa kasi
nimeona ninukuu vifungu hivi kwa rejea yake na wenye tabia kama yake.
Lakini matamshi hayo ni uthibitisho tosha kuwa Ndg. Lowassa, Chama chake
cha CHADEMA na vyama vinavyomuunga mkono chini ya UKAWA ni wabaguzi,
wachochezi na waroho wa madaraka wasiojali masilahi mapana ya nchi yetu.
Kwao madaraka ni muhimu kuliko nchi yetu.
Hii si mara ya kwanza kwa Ndg. Lowassa, Chama chake cha CHADEMA na
makada wenzake kutoa kauli na kufanya vitendo vya kibaguzi, kwa kutumia
ukanda na sasa wameamua kutumia udini kama njia ya mkato ya kutafuta
madaraka.
Chama Cha Mapinduzi kinaamini huu si msimamo wala utamaduni wa
Watanzania, bali ni uroho binafsi wa madaraka wa Ndg. Lowassa na chama
chake, hasa baada ya kuona kuwa hoja zake za kutafuta nafasi ya juu
kabisa ya uongozi wa nchi yetu zimekataliwa na wananchi.
Mwalimu aliwahi kutuonya juu ya wanasiasa wanaotumia udini na ukabila
kama hoja ya kutaka kupata madaraka kuwa ni wanasiasa walifilisika
kisiasa lakini ni watu wa hatari sana kwa mustakabali wa amani, umoja na
mshikamano wa nchi yetu.
Hivyo basi, Chama Cha Mapinduzi kinalaani kauli hii na tunaamini
inapaswa kulaaniwa na wote wanaoipenda nchi yetu. Lakini CCM inaamini
vyombo vinavyohusika na hasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itachukua hatua
zinazostahili kuondoa mbegu hii ya kansa inayoletwa na Ndg. Lowassa
kwenye nchi yetu. Maneno ya Ndg. Lowassa ni kansa mbaya kwa nchi yetu na
lazima yakemewe na kukomeshwa kabisa.
Maneno na vitendo vya Ndg. Lowassa, chama chake, na makada wenzake wa
CHADEMA na vyama shirika vya UKAWA toka wameanza kampeni katika maeneo
mbalimbali ya nchi yetu na kwa nyakati tofauti zimejaa ghiriba na
ubaguzi uliokithiri. Tabia hizi za Ndg. Lowassa ni moja ya sababu
iliyopelekea CCM kutompa nafasi ya kugombea kupitia Chama hichi.
CCM inatoa wito kwa wadau wote na Watanzania wote kuwa ni vizuri kuwa
makini wakati huu wa Uchaguzi, kuhakikisha hakuna jambo linaligawa Taifa
letu. Tuendeshe kampeni bila kuligawa na kuliangamiza Taifa letu.
Tanzania yetu ni muhimu. Tanzania kwanza mengine baadae.
Imetolewa na;-
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
08/09/2015credit:mpekuzi
Post a Comment