Lakini
mwenyekiti huyo wa Chadema amesema watu hao hawataki kutangazwa majina
yao kutokana na kuhofia kufuatiliwa na vyombo vya dola, akisema kitendo
hicho ni cha kushangaza kwa nchi huru kama Tanzania.
Chadema,
ambayo inashirikiana na NLD, CUF na NCCR Mageuzi chini ya mwamvuli wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) iliandaa harambee hiyo juzi kwenye
ukumbi wa Mlimani City kwa ajili ya kutafuta fedha za kuchangia shughuli
zao za kampeni zinazoendelea kote nchini.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na takriban watu 800, jumla ya Sh97 milioni zilikusanywa, ikiwa ni fedha taslimu, michango kwa njia ya simu na ahadi.
Baada ya kazi ya uchangishaji kuanza, Mbowe alishika kipaza sauti na kueleza michango mingine kutoka nje ya ukumbi huo.
“Wakati
tunaendelea na uchangiaji hapa, nimepokea simu kutoka kwa rafiki zangu
watano wenye uwezo mkubwa kiuchumi. Wameahidi kuchangia harambee lakini
wanaogopa kujulikana kwa kuhofia mkono wa serikali,” alisema mwenyekiti huyo.
“Inasikitisha
Mtanzania mwenye uhuru ndani ya Taifa lake anahofia kuchangia safari ya
mabadiliko kwa sababu ya kuiogopa Serikali, wakati Serikali iliyopo
imejaa mafisadi wakubwa?
“Unaweza
kuona hii ni Serikali ya namna gani, lakini ningewaomba niwatie moyo tu
ndugu zangu wenye nia ya mabadiliko, tuwe na ujasiri, msiogope.”
Sheria
ya Gharama za Uchaguzi, ambayo mwaka huu imeweka kiwango cha juu cha
matumizi ya kila chama kuwa Sh17 bilioni, inataka uwazi wa vyanzo vya
mapato na matumizi, lakini ni nadra kwa wafanyabiashara kuweka bayana
michango yao kwa vyama vya upinzani.
Chadema
imekuwa ikinufaika na michango ya fedha na mali kutoka kwa
mfanyabiashara maarufu nchini, Mustapha Sabodo, ambaye amekuwa
akitangaza hadharani kila anapokichangia chama hicho.
Alipoulizwa ni kiasi gani chama hicho kimepanga kutumia kwenye uchaguzi, Mbowe alisema ni vigumu kutaja.
“Uchaguzi
ni dynamic (unabadilikabadilika). Hesabu za siku haziwezi kuwa sawa
wakati wote. Kwa mfano bango la kupinga bao la mkono, inahitajika sana
kwa wakati huu lakini gharama inaweza kuwa nyingine wakati wa kusambaza
bango jingine,” alisema Mbowe.
Mkurugenzi
wa mipango na uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kila chama ndani
ya umoja huo kinajitegemea kwenye gharama za wagombea wake kwa ngazi ya
majimbo na udiwani.
“Hakuna
tathmini ya pamoja ya Ukawa...taarifa za gharama kwa CUF tutaziweka
wazi baada ya kukamilisha majumuisho ya taarifa zote kutoka majimboni na
ngazi ya madiwani,” alisema Mketo.
Akifungua
harambee hiyo, Mbowe alisema mikoa iliyosalia ni mingi kwa hivyo bado
wanategemea zaidi michango ya wadau katika kufanikisha kampeni.
Mbowe
alisema muda uliobakia ni wa “vita ya lala salama”, ambayo inahitaji
bajeti ya kutosha ili kufanikisha kufikia wapiga kura wengi
watakaoshiriki uchaguzi huo.
“Ukichangia
harambee hii hautakuwa umemchangia Mbowe au Lowassa, bali utakuwa
umechangia ufanikishaji wa kufikia ndoto ya mabadiliko. Utakuwa
umechangia ukombozi wa akina mama na vijana wa Taifa la Tanzania,” alisema Mbowe.
“Tangu
kuanza kwa kampeni hizi, Ukawa tumekuwa tukisaidiwa na Watanzania
mbalimbali wenye nafasi zao, wapo waliotoa usafiri wa magari ya kufanyia
kampeni. Kwa hivyo tunahitaji sana mchango wako katika kipindi hiki.”
Chadema
pamoja na Ukawa zimekuwa zikipambana sambamba na CCM kwenye kampeni za
urais na ubunge na matumizi yao makubwa yanaonekana kuwa katika gharama
za safari za wagombea, matangazo ya redio na televisheni, matangazo ya
moja kwa moja ya mikutano yao ya kampeni, posho za mawakala na vifaa
kama mavazi, bendera, vipeperushi na mabango.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo, mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, ambaye ni
pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, aliwataka waalikwa kuhakikisha
wanashiriki kikamilifu kuchangia harakati za mabadiliko ili kufanikisha
ndoto za kuwakomboa Watanzania kutoka mikononi mwa Serikali ya CCM.
Mwingine
aliyezungumza na waalikwa ni mgombea mwenza wa urais, Juma Duni Haji,
maarufu kwa jina la Babu Duni, ambaye alikuwa kivutio kutokana na
vijembe na misemo anayotoa wakati akiwa jukwani.
Duni alisema kutoa ni moyo na siyo utajiri kwani wapo wenye fedha nyingi, lakini hawana moyo wa utoaji.
Credit:Mpekuzi
Post a Comment