Lugha
hiyo chafu ambayo inajidhihirisha kwa matusi ya wazi, maneno ya
uchochezi, kashfa, kejeli, dharau na udhalilishaji wa kada mbalimbali za
kijamii wakiwemo viongozi wa kitaifa inaonesha wazi kulenga katika
kuigawa jamii na kufifisha amani, upendo, uzalendo na ustaarabu
tuliokuwa nao watanzania.
Ieleweke
kwamba kwa mujibu wa misingi ya Sanaa Duniani kote kazi zote za Sanaa
zinapaswa ziwe ni zenye kuonya, kuelimisha, kuadabisha, kukosoa,
kuburudisha, kuhamasisha na kuchochea maendeleo chanya katika jamii na
siyo kuigawa au kuivuruga jamii.
Ndiyo
maana msanii anayefanya kazi zake kwa kuzingatia misingi ya Sanaa
anatambuliwa kuwa ni kioo cha jamii, kiongozi na pia ni mwalimu wa yale
yote yaliyo mema katika jamii inayomzunguka.
Kinyume
na misingi hiyo ya Sanaa, baadhi ya Wasanii, studio za kurekodia na
kutengenezea muziki, vyombo vya habari vya kielektroniki na mitandao ya
kijamii ama kwa kutumiwa au kwa utashi wao binafsi wamekuwa
wakijihusisha na Sanaa zenye viashiria vya uchochezi na kuvunja misingi
ya weledi katika Sanaa hususan katika kipindi hiki cha kampeni na
maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Aidha,
baadhi ya Wasanii wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya vyama vya Siasa au
wagombea na kujikuta wakitumiwa vibaya na kuvunja misingi ya Sanaa kwa
faida za kisiasa. BASATA linapenda kutoa maagizo yafuatayo:
1.Wasanii
wana haki zote za kikatiba na kidemokrasia kushiriki shughuli za Siasa
lakini wanawajibika kwa kiwango cha hali ya juu kulinda misingi ya
weledi, maadili, miiko na hadhi yao kama inavyofanyika katika tasnia
zingine.
2.Wasanii
wanapaswa kutambua kwamba kuna maisha na Taifa baada ya uchaguzi mkuu.
Umoja wa kitaifa na umoja baina ya wasanii wa kada zote za Sanaa ndiyo
utakuwa msingi mkuu wa kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya Sekta
ya Sanaa na Taifa kwa ujumla pasipo kugawanyika katika misingi ya
itikadi za kisiasa
3.Wasanii
wasitumie nafasi na umaarufu wao kuligawa taifa, kukashifu viongozi wa
kitaifa, kudharau mamlaka, vyama na makundi mbalimbali katika jamii kwa
kile kinachoitwa ushabiki wa kisiasa. Ieleweke kuwa Serikali haitafumbia
macho wale wote watakovunja sheria, kanuni na taratibu. Tukumbuke kuwa
hakuna mtu aliye juu ya sheria.
4.Ijulikane
kuwa wasanii kama kundi muhimu katika kipindi cha kampeni za kisiasa ni
sawa na watu wengine wanaopewa kazi ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
Wasanii wasitumiwe kama vyombo tofauti na watu wengine.
BASATA
linatoa onyo kali kwa msanii yeyote atakayeendelea kukaidi, kuvunja
maadili na kusambaza kwa njia yoyote ile kazi ya Sanaa yenye ukengeufu
wa maadili.
BASATA
linawatakia wasanii wote utekelezaji mwema wa maagizo haya lakini kubwa
kuliko yote kutambua kwamba tunatakiwa kujenga mshikamano, umoja wa
kitaifa na kustawisha amani tuliyonayo ambapo ikitoweka itaathiri
ufanisi wa Wasanii na kuirejesha itatugharimu sana.
Sanaa itumike kulinda amani, kujenga upendo, umoja wa kitaifa na mshikamano baina ya makundi mbalimbali ya kijamii.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
Credit:Mpekuzi
Post a Comment