Ahadi za UKAWA zaitikisa Serikali

Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea kushika kasi, ahadi za mgombea urais Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa zimeanza kuichanganya Serikali na jana Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliibuka na kudai mgombea huyo anaahidi mambo ambayo tayari yanatekelezwa na Serikali ya CCM. Ahadi ambazo zimemshtua Sitta ni ile ya ujenzi wa reli mpya ya kati na kufufua shirika la ndege...Serikali (ATCL) alizozitoa Lowassa wakati wa uzinduzi wa kampeni zake.

Akizungumza na wanahabari jana, Sitta ambaye ni mjumbe katika timu ya kampeni ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli alisema amemsikia Lowassa akisema atajenga reli ya kati na kufufua ATCL, wakati Serikali ya CCM ilishaanza utekelezaji wa miradi hiyo.

Hata hivyo, wakati Sitta akisema Rais Jakaya Kikwete atazindua ujenzi wa reli hiyo kwa kiwango cha kimataifa itakayogharimu Dola 7.6 bilioni sawa na Sh16 trilioni, alisema mazungumzo kuhusu mkopo kutoka katika Benki ya Rolthschild ya Marekani kwa ajili ya ujenzi huo yanaendelea.

“Namshangaa Lowassa anasema atajenga reli na kufufua ATC wakati hii ni mipango ya Serikali ambayo ipo katika hatua za utekelezaji,” alisema.

Sitta alisema Rais Kikwete atazindua ujenzi wa reli hiyo Septemba 15, mwaka huu, katika eneo la Soga Mpiji wilayani Kisarawe.

Hivi ni mgombea gani wa urais ambaye hafahamu kuwa reli hii inajengwa na Kikwete, atafute mradi mwingine huu wa reli amechelewa,” alisema Sitta.

Alisema reli hiyo itakayokuwa na kilomita 2,561, itajengwa na Kampuni ya China Railways Construction Corporation kutoka Dar es Salaam – Kigoma, Tabora – Mwanza na Kaliua – Mpanda.

Mradi huo ukikamilika, utawezesha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa treni ya mwendo wa wastani wa kilomita 120 kwa saa.

Alisema reli hiyo ikikamilika, itakuza uchumi wa Tanzania na nchi za Maziwa Makuu za Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Alisema pamoja na kwamba kuna reli inayojengwa kutoka Mombasa, Kenya hadi Kigali, Rwanda baadhi ya nchi za Maziwa Makuu zitatumia reli ya Tanzania kwa sababu kijiografia kuna umbali mfupi. Alisema mradi huo utakaoanza mwaka huu, utakamilika mwaka 2021.

Pia, alisema itajengwa reli nyingine kutoka Mtwara hadi Mbambabay ili kuwezesha makaa ya mawe na chuma kusafirishwa hadi katika Bandari ya Hindi.

Kuhusu ATC
Akizungumzia ahadi ya shirika la ndege, Sitta alisema hata bila ahadi ya Lowassa, Serikali italifufua shirika hilo ili liweze kununua ndege nne na kuanza biashara kama ilivyokuwa zamani.

Alisema Serikali itachukua madeni yote ambayo shirika hilo linadaiwa ili liweze kukopesheka... “Unajua shirika likiwa na madeni haliwezi kupata mikopo,” alisema.

Alisema Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), italikopesha shirika hilo ili linunue ndege nne, Boeing mbili na Jet mbili. Alisema ndege hizo zitakuwa zikifanya safari za ndani na nje ya nchi na zitajiendesha na kurudisha madeni yake.

“Tunaendelea kuwalipa mishahara marubani wetu ili waendelee kuwa na sifa za kuendesha ndege mara zitakaponunuliwa,” alisema.

Waziri huyo wa Uchukuzi, aliahidi kuwa ndege hizo zitaanza kufanya kazi ndani ya miezi 12 kuanzia sasa.

Ufisadi TRL
Waziri Sitta pia alizungumzia ufisadi katika ununuzi wa mabehewa 274 ya Shirika la Reli Tanzania (TRL), kutoka India kuwa watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukamilisha kazi hiyo.

Sitta alikuwa akijibu hoja za Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyesema katika uzinduzi wa kampeni za Ukawa na Chadema kuwa mradi huo ni miongoni mwa matukio saba ya kifisadi yaliyotokea wakati Lowassa hayuko serikalini.

Hata hivyo, Sitta alisema: “Siwezi kufahamu ni lini watafikishwa mahakamani kwa kuwa suala hilo sasa liko mikononi mwa DPP, kazi yangu nilishaimaliza.”

Alisema kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo imeshakamilisha kazi yake na kuonyesha kwamba kulikuwa na uzembe kwa watendaji wa TRL uliosababisha kununuliwa kwa mabehewa hayo.

Alisema kamati hiyo ilikwenda hadi India kuichunguza kampuni iliyotengeneza mabehewa hayo na kubaini zabuni kuwa haikuwa na sifa na hivyo watendaji TRL walikiuka kanuni za ununuzi ya Serikali kwa kitendo cha kutoa fedha zote kwa kampuni hiyo kabla ya kupokea mabehewa.

Waliosimamishwa kutokana na sakata hilo ni Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomile Ngosomile, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi wa Ndani, Jasper Kisiraga na Meneja Mkuu wa Ununuzi Ferdinand Soka.

Azungumzia Richmond
Alipoulizwa sababu za kuibua upya suala la Richmond juzi kwenye kampeni Mjini Shinyanga wakati alishalifunga bungeni alipokuwa Spika, Sitta alisema hawezi kulizungumzia kwa kofia yake ya Waziri wa Uchukuzi akaahidi kufanya hivyo kwenye majukwaa ya siasa kwa kuwa yeye ni mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM.

Alisema pamoja na kuwa Serikali iliachiwa utekelezaji wa maazimio kuhusu kashfa hiyo, anapopanda kwenye majukwaa ya kisiasa lazima aeleze kile anachokifahamu kwa sababu anayetafutwa  hivi sasa ni mkuu wa nchi.

Kuhusu wizi wa kura, Sitta alisema Ukawa wanawaaminisha watu kwamba CCM itaiba kura, akihoji itaiba vipi wakati kila mgombea anakuwa na wakala katika kila kituo na kufafanua kuwa wanawaandaa wananchi kisaikolojia kukataa matokeo.


credit:Mpekuzi 

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright Enter Media Published.. Blogger Templates
Back To Top