Mkuranga. Majambazi watatu, wakiwa na silaha aina ya SMG, jana
asubuhi waliua askari mmoja na kujeruhi watu wengine wawili na baadaye
kupora bunduki na mamilioni ya fedha kwenye benki ya NMB, Tawi la
Mkuranga mkoani hapa.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya gari
kuwasili na makasha ya fedha, huku shughuli za utoaji huduma kwenye tawi
hilo zikiendelea.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Jafar Ibrahimu
alisema kuwa bado hajafahamu kiasi halisi cha fedha zilizoporwa kwani
alikuwa hajafika eneo la tukio.
Hata hivyo alisema askari aliyeuawa hakuwa mmoja
wa polisi waliokuwa lindo kwenye tawi hilo la NMB, bali alikuwa anapita
kuelekea kazini ndipo akakumbana na tukio hilo
Kamanda Ibrahim alibainisha kuwa taarifa ya awali
aliyonayo ni kwamba katika tukio hilo hakuna silaha wala risasi
iliyoporwa na majambazi hayo.
“Ndio ninakwenda eneo la tukio, kwani awali
ninaweza kusema kweli tukio la ujambazi limetokea hapo NMB na nimeelezwa
kuna askari kauawa, lakini si mmoja wa wale waliokuwapo lindoni,”
alisema Kamanda Ibrahim.
“Lakini pia hakuna silaha iliyoporwa,
zilizochukuliwa ni fedha ambazo bado haijafahamia ni kiasi gani na
ziliporwa zikiwa tayari zimefikishwa ndani ya ofisi hiyo. Askari
waliokuwa wamezisindikiza siyo polisi wetu bali ni wa kampuni binafsi,”
alisema Kamanda Ibrahim.
Alisema kwa sasa, polisi wa Wilaya ya Mkuranga,
Rufiji na Dar es Salaam wapo katika msako mkali kuwasaka watu
waliohusika katika tukio hilo la ujambazi.
Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa Wilaya ya
Mkuranga, Abdalah Kihato alisema majambazi hao waliokuwa watatu
walivamia benki wakati wafanyakazi wa benki hiyo wakiwa katika
maandalizi ya kupokea fedha hizo.
“Inaonekana majambazi hao walikuwa na taarifa za ujio wa fedha hizo kwenye benki hiyo,” alisema.
Alisema polisi mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi,
na kwa mujibu wa Kihato, polisi huyo alikuwa akijiandaa kuingia kazini
jana mchana, huku askari wawili waliokuwa zamu kituoni hapo
wakijeruhiwa kwa risasi.
Mwingine aliyejeruhiwa ni mtumishi mmoja wa benki
hiyo ambaye alipigwa panga. Wote wamehamishwa Hospitali ya Wilaya ya
Mkuranga kwa matibabu.
credited by Mwananchi Site
credited by Mwananchi Site
Post a Comment