TANZANIA imetajwa kuwa kinara katika nchi za Afrika Mashariki kwa kutunza amani na utulivu tangu ipate uhuru, huku Rais Jakaya Kikwete akiibuka kiongozi bora katika ukanda huo kwa kujitolea kuleta amani katika Bara la Afrika na kutunza amani hiyo nchini mwake.
Kwa
hali hiyo, Rais Kikwete ametunukiwa tuzo mbili na Taasisi ya East
Africa Book of Records ya nchini Uganda, moja ikiwa ni kwa ajili ya
Tanzania ambayo imefanikiwa kutunza amani pamoja na utulivu tangu uhuru
na nyingine ni ya Rais Kikwete mwenyewe kutokana na juhudi zake za
kupigania amani nchini mwake na eneo lote la ukanda wa mashariki mwa
Afrika.
Kutokana
na tuzo hizo, sasa Rais Kikwete ameacha kumbukumbu katika vitabu vya
nchi za Afrika Mashariki, kama mtu na kiongozi maarufu aliyetoa mchango
mkubwa katika kuleta amani kwenye nchi za ukanda huu.
Akikabidhi
tuzo hizo jana Ikulu, Dar es Salaam, Kiongozi wa taasisi hiyo Dk Paul
Bamutaze alisema wametoa tuzo hizo baada ya kuangalia mchango wa Rais
Kikwete katika kuleta amani katika baadhi ya nchi barani Afrika, akitoa
mfano namna kiongozi huyo alivyoleta amani mwaka 2008 nchini Kenya,
kufuatia machafuko baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
“Tuzo
ya kwanza tunaitoa kwa Tanzania kama nchi kwani ndio nchi pekee katika
eneo la Afrika Mashariki ambayo imedumisha amani na utulivu tangu kupata
uhuru na ndio imekuwa inasaidia kutatua migogoro mbalimbali kwa
majirani zake na inaendeshwa kwa utawala wa sheria,” alisema Dk Bamutaze.
Alisema
tuzo ya pili wanamkabidhi Rais Kikwete kutokana na kuwa kiongozi bora,
ambaye amedumisha amani nchini mwake, lakini pia ameshiriki kutatua
migororo mbalimbali.
Alisema licha ya Kenya, lakini ni Rais Kikwete ambaye ameshiriki kuleta amani nchini Burundi na kurejesha serikali iliyokuwepo madarakani baada ya kuwepo jaribio la uasi.
Alisema licha ya Kenya, lakini ni Rais Kikwete ambaye ameshiriki kuleta amani nchini Burundi na kurejesha serikali iliyokuwepo madarakani baada ya kuwepo jaribio la uasi.
Rais
Kikwete pia amesaidia kuleta amani katika nchi za Sudan Kusini, Comoro,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya Jeshi la Tanzania
kuwasambaratisha kundi la waasi la M23.
Mkuu
wa Kitengo cha Utafiti wa taasisi hiyo, Adam Buyinza alisema katika
utafiti ambao wameufanya, wamegundua kuwa Tanzania imedumu kuwa na amani
kutokana na kuongozwa na CCM ambacho kina sera zinazoeleweka.
Kwa
upande wake, Rais Kikwete alisema kwamba misingi ya amani na utulivu
uliopo nchini umewekewa misingi yake na Mwalimu Julius Nyerere, ambaye
uongozi wake haukubagua watu kwa misingi ya kidini, rangi na kabila au
eneo ambako anatoka mtu.
Alisema
tuzo hiyo aliyoipokea sio yake peke yake, bali ni ya wananchi wa
Tanzania pamoja na wasaidizi wake ambao yeye kama nahodha wa meli
wamesaidiana kuhakikisha kuwa meli yao inaenda vizuri hata pale
panapotokea mawimbi wanasaidiana kukiendesha chombo hicho.
Rais
Kikwete alisema kuwepo kwa amani nchini, kumetokana na watu wake
kuamini kwenye majadiliano badala ya kupigana na alisema hata pale
ilipotokea tofauti kati ya Serikali na vyama vya upinzani, walikaa meza
moja wakazungumza na pale ilipotokea tofauti kati ya Waislamu na
Wakristo pia walitatua migogoro yao kwa mazungumzo.
“Kwa
mfano kulitokea ugomvi wa nani ana uhalali wa kuchinja, haya mambo
walitaka mimi niingilie kati, lakini jamii yenyewe walikaa na
kujadiliana kwamba yametoka wapi na nani ameyachochea, walipokaa
waligundua kwamba hakuna faida kwani mambo hayo wamejiwekea jamii
husika,” alisema Rais Kikwete.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema
kwamba tuzo hizo alizotunukiwa Rais Kikwete ni kitu kikubwa kwa Rais
anayeondoka madarakani.
credit:Mpekuzi
Post a Comment