Kauli
ya Mbowe inakuja siku mbili baada ya Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
Leticia Ghati Musore na katibu mkuu wa chama hicho Mosena Nyambabe
kudai kwamba “Chadema imejipa umiliki wa UKAWA.”
Wakizungumza
mbele ya waandishi wa habari viongozi hao wa NCCR-Mageuzi walimtuhumu
mwenyekiti wao James Mbatia ‘kutekwa’ na Chadema na kwamba, ameshindwa
kukitetea chama chao kwa kile walichosema kumezwa katika umoja huo.
Akizungumza
na waandishi jana, Mbowe alisema viongozi hao wana jambo lingine nje ya
yale waliyoyatamka hadharani na kwamba, kubwa ni kutaka kupewa
upendeleo wa kugombea majimbo licha ya kukosa sifa.
“Tulikubaliana
kuwa ili chama kipewe jimbo tutaangalia matokeo ya chama 2010,
tutaangalia madiwani wa chama husika katika jimbo, mtandao wa chama pia
matokeo ya uchaguzi wa vijiji na mitaa 2014 pamoja na mtandao wa ushindi
wa mgombea” alisema Mbowe.
Mbowe
alisema majimbo ambayo Nyambabe na Leticia wamekuwa wakiyang’ang’aniwa
kugombea licha ya kutokuwa na sifa ni Segerea la jijini Dar es Salaam
ambalo walipewa CUF na Jimbo la Serengeti lililopo Mara ambalo
limekabidhiwa kwa Chadema.
“Nyambabe
alihitaji kugombea Jimbo la Serengeti ambako Chadema ilishinda vijiji
38 lakini NCCR haikushinda hata kijiji kimoja katika uchaguzi wa vijiji,
Chadema ina madiwani 8 NCCR haina hata mmoja, Nyambabe amegombea jimbo
hilo mara mbili kwa vyama tofauti lakini hakupata hata asilimia 5,
tungempaje hapo?” alihoji Mbowe.
Kwa
upande wa Musore, Mbowe alieleza kwamba mwanamama huyo aliomba aachiwe
kugombea katika Jimbo la Segerea ambako NCCR haina mtandao wa ushindi
wala nguvu “jambo hili UKAWA tulilipinga.”
“Musore
tunamfahamu aliwahi kuwa diwani wetu Tarime, hakujijenga wala kujenga
NCCR, katika Jimbo la Segerea pia lakini akawa anataka tumzawadie jimbo
kama makamu mwenyekiti taifa, hapana! tunataka kushinda hatuwezi kufanya
uamuzi tunaojua wananchi wataukataa,” alisema Mbowe.
Hata
hivyo alisema UKAWA bado wanaendelea na utatuzi wa migogoro
iliyojitokeza katika majimbo na kwamba mambo yatakuwa mazuri muda si
mrefu.
“Huu
ni muungano wa vyama vinne, lazima kutofautiana kuwepo lakini kamwe
hatuwezi kushindwa kuelewana katika maeneo machache yaliyobaki na hivi
tunavyoongea Profesa Baregu, Salum Mwalimu, Bashage na viongozi wa CUF
taifa wameelekea majimbo yenye shida,” alisema Mbowe.
Baadhi ya majimbo yaliyo na utata ni Mtwara Mjini, Kigamboni, Itilima (Simiyu), Masasi, Mtama (Lindi), Ngara na Sikonge.
Msikilize Mbowe akiongea
Msikilize Mbowe akiongea
Credit:Mpekuzi
Post a Comment