Tuesday, September 15, 2015 LOWASSA: Nitaanzisha Benki ya Mama Lishe na Bodaboda ili Kufuta Umasikini

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CHADEMA na UKAWA, Edward Lowassa, ameahidi kuanzisha benki maalumu ya  kusaidia mamalishe, waendesha pikipiki za bodaboda,  wajasiriamali wadogo ili waweze kupata mikopo na kukuza vipato vyao.
 
Bw. Lowassa aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Stendi Mjini Kahama, mkoani Shinyangana kuongeza kuwa, akiingia Ikulu ataifanya wilaya hiyo kuwa mkoa. 
 
Alisema wachimbaji wadogo wa dhahabu mkoani humo wamekuwa wakinyanyaswa na kunyang'anywa maeneo ya uchimbaji; hivyo akiwa Rais, wazawa watapewa fursa kubwa ya kuchimba dhahabu pamoja na kupewa maeneo ya kufanyia kazi hiyo. 
 
"Nimechoka na umaskini, nitahakikisha naboresha mazingira ya kilimo na kuanzisha soko huria ili wakulima wanapolima mazao yao wayauze popote ikiwemo nje ya nchi bila ushuru.
 
"Sijawahi kuona Serikali legelege kama ya CCM, naomba mnipe kura nyingi niweze kuwa rais, Serikali ambayo nitaiunda itakuwa rafiki wa watu maskini, mamalishe, waendesha pikipiki za bodaboda na wachimbaji wadogo ili nichochee maendeleo," alisema. 
 
Awali aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani humo ambaye alihamia CHADEMA, Hamisi Mgeja, alisema Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi zake katika mkoa huo.
 
Alisema aliahidi kupeleka umeme wa uhakika mjini Kahama, kujenga Kiwanda cha Nyama, Uwanja wa Ndege, kuongeza mtandao wa maji ahadi hizo hadi leo hajazitekeleza.
 
Naye mgombea ubunge Jimbo la Kahama kwa tiketi ya CHADEMA,Bw. James Lembeli, alimkabidhi Bw. Lowassa mfano wa ufunguo akimtaka autumie kufungua makufuli yote katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu.




Credit:Mpekuzi

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright Enter Media Published.. Blogger Templates
Back To Top