Sikuamini
masikio yangu kwamba haya ni maneno yaliyotoka kinywani mwa mgombea
urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Pombe Magufuli.
Alikuwa
akiongea na wananchi wa Tanga katika mkutano wa kampeni akiwahadharisha
Watanzania wasivichague vyama vya upinzani, kwa lengo la kufanya
mabadiliko kwa sababu kufanya hivyo ni kuchagua bora mabadiliko wakati
mabadiliko bora yatapatikana.
Nia
yangu siyo kumfedhehesha mgombea huyu anayesifika kwa uadilifu na
uchapakazi, lakini hivi kuna asiyejua kuwa Saddam Hussein hakuwa rais wa
Kuwait bali Iraq? Kila mtu anajua hivyo, nashangaa tu kwamba mgombea
wangu wa urais ama kweli hajui hili au hayuko makini katika masuala ya
kimataifa.
Ninachokusudia
ni kujaribu kuwahadharisha Watanzania kwamba zama hizi rais wa nchi
haongozi ndani ya mipaka ya nchi hiyo pekee, bali anakuwa kiungo muhimu
kati ya nchi yake na jamii ya kimataifa katika ulimwengu huu ambao sasa
ni kama kijiji.
Moja
ya mafanikio ya rais wa nchi yeyote ile duniani ni jinsi gani
anazicheza karata zake kwenye medani ya kimataifa. Siasa za kimataifa
siku hizi ni mchezo hatari, kiasi kwamba kama rais hazijui vizuri siasa
za kimataifa kuna hatari ya kushindwa kutekeleza ilani na sera za chama
chake awapo madarakani, kwa sababu ya misuguano na wale waitwao
washirika wa maendeleo ambao ni nchi zilizoendelea.
Ukubwa
wa hatari hii unazidi pale nchi yetu inapoingia katika uchumi wa mafuta
na gesi asilia. Rasilimali mbili hizi zimeyaingiza mataifa yenye
rasilimali hizo katika machafuko.
Kwa
mujibu wa andiko, Oil and Diamonds as causes of civil war in
sub-Saharan Africa, rasilimali ya mafuta na gesi zinaweza kuitia nchi
katika machafuko. Lakini hilo hutegemea wingi wa rasilimali hiyo, sera
na mikataba ya nchi husika kwa mataifa na mashirika wahitaji wa
rasilimali hiyo kwa lugha rahisi wawekezaji.
Jingine
ni uwezo wa kidiplomasia ya uchumi wa viongozi wa nchi yenye rasilimali
kumudu hila, njama, migandamizo na vishawishi vya wawekezaji hao. Kwa
maneno mengine, uwezo wa rais aliye madarakani katika kuongoza
diplomasia na mataifa ya nje.
Mbali
na rasilimali, uwezo wa rais katika diplomasia na mataifa ya nje ni
mtaji muhimu katika kuvutia wawekezaji katika kile kijulikanacho kama
mitaji ya moja kwa moja kutoka nje au ‘foreign direct investment (FDI)’,
misaada mbalimbali kwa nchi na hata haiba ya nchi kimataifa.
Kwa
kweli Rais wa Tanzania anayemaliza muda wake ameipaisha Tanzania katika
medani ya kimataifa, ingawa mwishoni mwa utawala wake mataifa na wadau
wa maendeleo walifikia kuzuia misaada yao kupinga kashfa mbalimbali,
ikiwamo kashfa ya Tegeta Escrow iliyolitikisa Taifa.
Hatari
iliyoko mkipata rais asiyejua changamoto zinazolikabili taifa katika
siasa za kimataifa ni kuchukua maamuzi yanayoweza kuliingiza taifa
katika hasara na hata katika migogoro ya ndani na nje.
John
Perkins anaandika katika kitabu chake “The confession of an economic
hitman” kwamba mashirika ya kimataifa hususan yale ya uchimbaji mafuta
na gesi, huyaingiza mataifa katika lindi la madeni, umaskini na vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
Hapo ndipo unapoonekana umuhimu wa kuwapima wagombea wetu ili kuona ni nani anafaa kwa siasa za nje?
Mwandishi wa makala katika gazeti mmoja litokalo kila siku hapa nchini, alimsifia Dk John Magufuli kwamba katika kipindi chake cha miaka 20 ya utumishi serikalini, amesafiri kwenda nje ya nchi mara nne !
Mwandishi wa makala katika gazeti mmoja litokalo kila siku hapa nchini, alimsifia Dk John Magufuli kwamba katika kipindi chake cha miaka 20 ya utumishi serikalini, amesafiri kwenda nje ya nchi mara nne !
Hii
inaonyesha kuwa si mtu mbadhirifu kwani uchache wa safari za nje
unathibitisha kuwa yeye siyo mwenye kufanya matumizi ya ovyo ovyo. Japo
hili ni jambo zuri kwa upande mmoja, kwa upande wa kukuza uelewa wake
katika medani za kimataifa, si jambo la kujivunia. Ziara za nje hupanua
uelewa wa mtu katika diplomasia ya kimataifa.
Magufuli Vs Lowassa
Kupitia
hotuba zake za kampeni mtu anaweza kupata wasiwasi juu ya uwezo wa Dk
Magufuli kuhusu siasa za nje. Ule mfano wake maarufu wa kulinganisha
mabadiliko ya Tanzania na yale yaliyotokea Libya umetoa picha hasi
kwamba hajui vyema siasa za kimataifa.
Ukichanganya
na kauli yake “mimi sifanyagi (sifanyi) siasa na kwa bahati mbaya
naweza kuwa si mwanasiasa mzuri,” unapata shaka kama kweli atamudu siasa
za kimataifa zilizojaa ulaghai, hila na mizengwe dhidi ya nchi changa.
Ili kuwa rais zama hizi, inabidi uzijue vizuri siyo siasa za ndani bali
hata zile za kimataifa.
Hili
la kutokujua au kujichanganya kuhusu Saddam alikuwa rais wa nchi gani
linaweza kuonekana jambo dogo, lakini kwa watu makini haiwezekani kwa
mtu msomi wa kiwango cha uzamili tena aliyekuwa katika uongozi wa nchi
kama waziri kwa muda mrefu, awe hajui Saddam alikuwa rais wa nchi gani.
Ni dalili kwamba kuna upungufu mkubwa kwenye uelewa wa mambo ya
kimataifa kwa mgombea wetu huyu.
Lowassa
kwa upande wake hatujamsikia akizungumzia lolote kuhusu masuala ya
kimataifa, licha ya kuwa amewahi kuwa Waziri Mkuu na waziri wa kawaida
kwa miaka mingi.
Nafasi
hiyo bila shaka ilimpa uzoefu fulani katika medani ya kimataifa, kwa
kuwa Waziri Mkuu ni msaidizi wa karibu wa rais kwenye mambo yote
likiwamo la ushirikiano wa kimataifa. Aidha, Lowassa amesafiri mara
nyingi nje ya nchi jambo linalompa fursa ya uelewa mpana kuhusu masuala
ya nchi za nje.
Katika
kampeni zake, tumemsikia akisema “sitosubiri misaada kutoka nje”. Hii
ni kauli nzito kwa kuwa nchi hizi changa kama Tanzania haziwezi kabisa
kuepuka misaada kutoka nje, ingawa pia hazitakiwi kuwa tegemezi kwani
zina rasilimali nyingi.
Kuwa
kwake Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC),
bila shaka kulimwezesha kukutana na wanadiplomasia wengi wa kimataifa
wakiwamo mabalozi, mawaziri wakuu, makamu wa marais na hata marais
waliowahi kuhudhuria mikutano ya kimataifa katika ukumbi huo.
Tukumbuke
kwamba, mchakato wa Ushirikiano wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki,
utakuwa unaingia katika kipindi nyeti cha ushuru wa pamoja wa forodha
na mamabo mengine ambapo masilahi ya nchi yetu itabidi yalindwe
ipasavyo.
Ni
wazi marais wa nchi jirani wanasubiri kwa hamu ni nani ataibuka Rais wa
Tanzania, nchi ambayo ‘kistratejia’ imekaa vizuri kuliko nchi zote za
Afrika Mashariki, lakini isiyokuwa na mikakati mizuri ya kufaidika na
uwepo wake kijiografia.
Mataifa
na mashirika ya nje kama vile Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na
mengineyo yatakuwa yanafuatilia kwa karibu uchaguzi wa Tanzania. Kwa
hiyo wakati tukishangilia kauli za wagombea kuhusu jinsi
watakavyoendesha siasa za ndani ya nchi, tusisahau kuna siasa za
kimataifa ambazo zinaweza kukwamisha hata mipango yetu ya maendeleo,
iwapo rais atakayechaguliwa hatokuwa na uzoefu au uelewa wa kutosha.
Mwandishi:Mpunta Wadinya; dinyampuntaz@yahoo.com
Mwandishi:Mpunta Wadinya; dinyampuntaz@yahoo.com
Credit:Mpekuzi
Post a Comment