WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, yuko mbioni kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ingawa sasa kinachosubiriwa ni kukamilika kwa masuala yanayoelezwa kuwa ya kiufundi, kabla ya kutangazwa kwa jambo hilo.
Raia Mwema linafahamu kwamba kuna masuala makubwa matatu yaliyosababisha hadi sasa isiwe imetangazwa kuwa Lowassa amejiunga na chama hicho kinara miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Gazeti hili limeambiwa na vyanzo vyake kutoka miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaofahamika kumuunga mkono Lowassa na Ukawa kuwa mbunge huyo wa Monduli ametaka Chama cha ACT-Wazalendo ambacho hakimo ndani ya Ukawa nacho kijumuishwe.
Lowassa anaelezwa kupendelea kuwa na Zitto endapo atajiunga na Ukawa kwa sababu kubwa tatu; ambazo ni ujana (umri), eneo analotoka na umoja wa wapinzani.
“Maono ya Lowassa ni kwamba kwa sababu wengi wa wapiga kura ni vijana, anahitaji mtu kama Zitto ili abebe matumaini ya kundi hilo. Si vizuri yeye ambaye ana umri wa miaka zaidi ya 60 akawa na Waziri Mkuu mwenye umri kama wake.
“Pili, Lowassa amesema anamtaka Zitto kwa sababu tofauti na Freeman Mbowe na Dk. Wilbrod Slaa ambao wanatoka Kaskazini mwa Tanzania kama yeye, kiongozi huyo wa ACT anatokea mkoani Kigoma. Nchi yetu sasa ni vigumu kutaka kuunda serikali halafu ukaonekana una watu kutoka upande mmoja wa nchi.
“Jambo jingine ambalo ni sababu ya tatu ya kuwa na Zitto ni umoja katika upinzani. Lowassa anataka vyama vyote vya upinzani viwe kitu kimoja na ndiyo maana anataka ACT nayo iingie kwenye Ukawa,” kilisema chanzo cha Raia Mwema kilicho ndani ya mazungumzo ya kutaka Lowassa aingie Ukawa.
Lowassa anadaiwa kutopendelea Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Waziri Mkuu wake endapo Ukawa itashinda kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa vile, kama ilivyo kwa Mbowe na Dk. Slaa, ana umri mkubwa ambao hautawavutia vijana wanaotaka kupigia kura mabadiliko.
Hata hivyo, matakwa hayo ya Lowassa yamedaiwa kuiweka Chadema katika wakati mgumu, kwa sababu suala hilo linakumbana na ukakasi katika eneo zaidi ya moja.
Kwanza, gazeti hili limeambiwa, wapo wana Chadema ambao hawakubaliani moja kwa moja na kitendo cha Lowassa –ambaye chama hicho kimewahi kumtangaza kama fisadi, kuwa mgombea wake wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kundi hilo la wana Chadema linadaiwa kuongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa na Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika huku Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, naye akitajwa kuwamo.
Taarifa hizi zinakwenda mbali kwa kusema kuwa Dk. Slaa amefikia hatua ya kutishia kuwa kama Lowassa atapitishwa kuwa mgombea wa Ukawa, yeye anaweza hata kufikia uamuzi wa kuhama Chadema na kurejea CCM.
Katika hao wanaotajwa kumpinga Lowassa, ni Lissu pekee ambaye amezungumza hadharani na kusema kwamba haamini kama mwanasiasa huyo ana “ubavu” wa kuhama CCM na kwamba hata kama atahama, haitakuwa rahisi kupitishwa kuwa mgombea kupitia Ukawa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anaongoza wana Chadema walio tayari kumpokea Lowassa. Miongoni mwa wanaomuunga mkono wanatajwa kuwa mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Suzanne Lyimo.
Pili, wanachama hao bado wanaamini kuwa Dk. Slaa ndiye mtu sahihi kushindana na Dk. John Magufuli ambaye amepitishwa na CCM kuwania urais na tatu wako wana Chadema ambao bado wana kinyongo na Zitto Kabwe kutokana na historia ya nyuma baina yao.
Kama ombi hilo la Lowassa litapitishwa, maana yake ni kwamba Zitto atatakiwa kupewa wadhifa wa Waziri Mkuu kivuli (Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni) endapo Ukawa haitashinda na hivyo kuwaongoza Mbowe na Dk. Slaa wanaoweza kulazimika kuomba ubunge.
Hali ilivyo CUF
Wakati kukiwa kumegubikwa na siri kuhusu ni nini hasa kinaendelea kwenye suala la kutafuta mgombea miongoni mwa vyama vilivyo kwenye Ukawa, Raia Mwema limeambiwa kuwa ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) kuna wanaokubali suala hilo na wasiokubali.
Kimsingi, gazeti hili linafahamu kuwa miongoni mwa sababu zilizofanya mazungumzo kusitishwa bila mwafaka wiki iliyopita, ilikuwa ni hofu ya CUF kuwa huenda Chadema itamsimamisha Lowassa.
“Chadema walikuwa wanataka wao ndiyo wapewe nafasi ya kusimamisha mgombea urais. Sasa tukawauliza, tuwaachie kwani mgombea wenu ni nani? Sisi mgombea wetu ni Profesa Ibrahim Lipumba sasa nyinyi wenzetu wenu ni nani?
“Wakatuambia wakimaliza mchakato wao wa ndani watamtangaza mgombea wao. Lakini sisi tuna taarifa kuwa Lowassa anazungumza na Chadema. Sisi CUF suala la Lowassa hatujalijadili, sasa wakimpitisha na sisi hatujui lolote itakuaje?”, alisema mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina.
Kiongozi huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba CUF Zanzibar haina shida kama Lowassa atahamia Ukawa au la lakini tatizo kubwa linaonekana kuwa kwa wanachama wa chama hicho upande wa Bara.
Raia Mwema limeambiwa na kiongozi huyo kutoka Bara kuwa kama Lowassa atahamia Ukawa kupitia Chadema na kuwa mgombea, huo ndio utakuwa mwisho wa CUF kama chama cha siasa kwa upande wa Bara.
“Sisi tunasema, kama Lowassa atahamia Chadema, sisi tutoke Ukawa na twende kuungana na chama kama ACT- Wazalendo kama hakitaingia kwenye huo mkumbo wa Lowassa. Kwa namna hiyo CUF itabaki na identity (utambulisho) yake na Chadema wataendelea na kazi ya kumsafisha Lowassa,” alisema.
ACT-Wazalendo
Akizungumza kuhusu uamuzi wa kujiunga na Ukawa, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote ambayo yamefanyika kuhusu wao kujiunga na ACT.
“Sisi tuliandika barua ya kuomba kujiunga na Ukawa huko nyuma lakini hatukujibiwa. Kwa sasa tunajipanga kuingia kwenye uchaguzi na tutashirikiana na chama chochote cha upinzani ambacho tunafanana kimtazamo.
“ Tangu Lowassa akatwe kwenye urais CCM, sijawahi kuzungumza naye wala kukutana naye na hivyo sijui hizo habari za ACT kuingizwa kweye Ukawa zinatoka wapi. Kama hilo jambo lingekuwapo, mimi ningekuwa najua lakini hadi unavyoniuliza mimi sijui lolote.
“ Hilo suala la Uwaziri Mkuu siwezi kulizungumzia kwa sababu halijafika kwenye chama changu na ndiyo nalisikia kutoka kwako. Likifika tunaweza kulizungumzia,”alisema.
Raia Mwema halikuweza kumpata Lowassa kuzungumzia kuhusu taarifa hizi kwa vile wakati tunakwenda mitamboni alikuwa safarini nje ya nchi.
Lowassa anahama au anabaki?
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka, ameliambia gazeti hili kuwa kwa namna anavyomfahamu Lowassa, si rahisi kwa mwanasiasa huyo kuhama CCM kwenda upinzani.
“Nimemfahamu kwa miaka mingi. Kwa sababu hiyo naweza kusema kuwa sidhani kama anaweza kuondoka CCM. Lowassa si mtu wa kuchezea rehani vitu na kwake kuhama CCM ni kucheza kamari. Simuoni akicheza kamari hiyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge ambao wamejitambulisha kuwa wafuasi wa Lowassa wamechukua fomu kuwania ubunge kupitia CCM ingawa taarifa za Waziri Mkuu wa zamani huyo kutaka kuhama zikiwa zinafahamika.
Baadhi ya wanachama hao ni Hussein Bashe, Nazir Karamagi, Lawrance Masha, Profesa Anna Tibaijuka, Mussa Azzan na wengineo ambao wamechukua fomu za ubunge.
Hatua hiyo imezua hofu ya kuwapo kwa hujuma kwa CCM endapo wanachama hao watapitishwa na kuamua kuhamia upinzani kumfuata Lowassa kabla ya uchaguzi; jambo litakalokifanya chama hicho kukosa wagombea.
Hata hivyo, watafiti wengine wanadai kuwa huenda hatua hiyo ya wana CCM ni ishara kwamba Lowassa hatahama chama hicho.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa hapa nchini, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kwake suala lililobaki si kwamba Lowassa anaweza kuhama CCM bali ni endapo atakubali kuwania urais kupitia Ukawa au la.
“Ninachoweza kukiona ni kwamba CCM itaathirika kama Lowassa ataondoka. Tofauti kubwa kati yake na Augustine Mrema ni kwamba yeye ataondoka na kundi la wanasiasa na hivyo mtikisiko wake utakuwa mkubwa zaidi.
“Anaweza asishinde urais mwaka huu lakini atakuwa amesaidia sana kukuza upinzani na naona kuwa kama atahama, upinzani utakuwa na nafasi nzuri zaidi mwaka 2020 kutokana na uamuzi wake huo,” alisema. - See more at: http://www.raiamwema.co.tz/lowassa-ukawa-ngoma-nzito#sthash.mKvwHkl7.dpu
credited by Raia Mwema

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright Enter Media Published.. Blogger Templates
Back To Top